Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema kiasi cha Bilion 71.7 za Kitanzania zitatumika kuiunganisha Uganda na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kipindi cha miaka 15. Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa Hafla ya Utiaji Saini Makubaliano ya Kibiashara ya Kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Uganda (NBI) iliyofanyika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, leo Septemba 29, 2023. “Leo hii tumeshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano – NICTBB na Mkongo wa Mawasiliano wa Uganda. Mkataba huu una thamani ya kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 28 sawa na fedha za Kitanzania Shilingi Bilion 71.7 kwa kipindi cha miaka 15. Mikongo hii itaunganishwa kupitia mpaka wa Tanzania na Uganda, eneo la Mutukula katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.” Amesema Waziri Nape. “Ni matumaini yetu, kuona Afrika ya Kidigital (Africa Digital) inafikiwa na matokeo yake chanya yanasaidia katika kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi na shughuli za kijamii barani Afrika kwa kutumia teknolojia. Ni matumani yetu kuona Afrika yenye mifumo imara ya Serikali Mtandao, Elimu Mtandao, Afya Mtandao, Biashara Mtandao, Kilimo Mtandao katika kutoa huduma kwa wananchi wetu.” Amesema Waziri Nape Aidha, Waziri Nape ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika kusimamia vyema kutoa huduma kwa mujibu masharti yaliyopo kwenye mkataba wa makubaliano. “Tuhakikishe tunatoa huduma bora na yenye uhakika, panapotokea changamoto yoyote ile iweze kushughulikiwa kwa haraka. Uganda inategemea huduma bora kutoka kwenu, mkatoe huduma yenye ubora kwa kuzingatia makubaliano ya Waheshimiwa Ma-Rais wetu. Kwa changamoto ambazo zitakuwa nje ya uwezo wenu, mziwasilishe Wizarani kupata ufumbuzi wa haraka”. Amesema Waziri Nape Katika hatua nyingine, Waziri Nape amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania, Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Peter Ulanga na Dkt. Hatwib Mugasa Mkurugenzi Mtendaji wa NITA-U kwa kubeba jambo hili kwa uzito wake na kufanikisha kuungaisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Tanzania –NICTBB na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Uganda unaosimamiwa na NITA-U. Mkataba huo umetokana mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kikazi nchini Uganda, ambapo yeye na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoel Kaguta Museveni walikubaliana kuunganisha miundombinu mikuu ya mawasiliano ili kuiwezesha Uganda na nchi jirani kupata huduma za intaneti zenye ubora na bei nafuu na pia kuunganisha nchi ya Uganda na mikongo ya baharini iliyopo Tanzania.
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ) Kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (SJMT) imeandaa Mkutano wa Wadau kuhusu tamko la Amri ya Waziri kuhusu CII na miongozo yake pamoja na mapendekezo ya uridhiwaji wa Mkataba wa Malabo Inayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Shirika la Bima Zanzibar, 29-30 Septemba, 2023. Ndg, Mahfoudh Mohamed Hassan Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi amefungua Mkutano huo Kwa niaba ya Katibu Mkuu WUMU (SMZ), ameeleza kuwa Warsha hii inawaleta pamoja Wadau muhimu sana katika Sekta ya TEHAMa Kwa ajili ya kupata uelewa wa pamoja na baadae kukusanya maoni Kwa upande wa Zanzibar . Aidha, amewaeleza Wajumbe kuwa chimbuko la Miundombinu Muhimu ya TEHAMA na Miongozo yake linatokana na hitaji la kutekeleza Sheria ya Makosa ya Mtandao ( Cybercrimes Act ) ya mwaka 2015 katika Kifungu Cha 28 ambacho kinampa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Mawasiliano uwezo wa Kutambua na Kutangaza Miundombinu muhimu ya TEHEMA (Critical Information Infrastructure - CII) pamoja na miongozo yake. Lengo la kuwepo Kwa Kifungu hiki katika Sheria tajwa ni kuweka nguvu za Kisheria za utambuzi wa Miundombinu muhimu ya TEHAMA Nchini Ili iweze kupewa ulinzi mkubwa na kuhakikisha kuwa huduma za msingi kwa Wananchi zinapatikana. ' Niwaombe sote tushiriki Katika uelimishaji huu kwa makini Ili kuwezesha utoaji wa maoni katika Rasimu ya Tamko la Amri ya Waziri kuhusu Miundombinu muhimu ya TEHAMA na katika mapendekezo ya Uridhiwaji wa Mkataba wa Malabo Ili kuwezesha Wizara zetu kutimiza wajibu katika ujenzi wa Taifa letu' Mkutano huu Umeudhuriwa na Menejimenti ya WUMU, Wakuu wa Taasisi Chini ya WUMU, Viongozi wengine kutoka Taasisi ya WUMU, Wawezeshaji na Watumishi kutoka WHMTH, Watumishi kutoka SMZ, Waandishi wa Habari pamoja na Ndugu Waalikwa.
Tarehe 28 Septemba,2023 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekutana na Wadau wa Habari kupitia kwa pamoja na kutoa maoni kuhusu rasimu ya sera ya Taifa ya TEHAMA. Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajukumu la kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera ya TEHAMA nchini. Kwa jukumu hilo Wizara iliweza kuanda mkutano huo na Wadau waweze kutoa maoni namna ya sera hiyo itakavyoleta mabadiliko chanya kwa Taifa. Sera hii itaweza kujenga na kulinda usalama wa Wadau na watu wengine katika jamii Kikao hicho kimehudhiriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara pamoja na watumishi wa Wizara na Wadau wa Habari.